Aliyekua Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Ubelgiji Roberto Martinez anatajwa kuwa kwenye mpango wa kukabidhiwa jukumu la kukiongoza kikosi cha Timu ya Taifa ya Ureno.
Taarifa kutoka nchini Ureno zinaeleza kuwa, Kocha huyo kutoka nchini Hispania yupo katika mzungumzo na Shirikisho la Soka la FPF.
Uongozi wa FPF umeanza mchakato huo baada ya kusitisha mkataba wa Kocha Fernando Santos, ambaye alishindwa kufikia malengo ya kufanya vizuri wakati wa Fainali za Kombe la Dunia 2022, zilizofanyika Qatar.
Ureno iliondolewa kwenye Fainali hizo, katika hatua ya Robo Fainali kufuatia kufungwa 1-0 na Timu ya Taifa ya Morocco.
Martinez anatajwa kuwa mbioni kukabidhiwa jukumu huko nchini Ureno, ikiwa ni majuma kadhaa baada ya kuachia nafasi ya Kocha Mkuu wa Ubelgiji baada ya Fainali za Kombe la Dunia, ambapo kikosi chake kiliishia hatua ya Makundi.
Kocha huyo aliyewahi kuvinoa vikosi vya Klabu za Everton na Wigan zote za England, alitajwa kuwa Kocha Mkuu wa Ubelgiji mwaka 2016, aliachana na timu hiyo kufuatia mkataba wake kufikia kikomo mwishoni mwa mwaka 2022.
Mafanikio makubwa ya Martinez ni kuiwezesha Ubelgiji kumaliza katika nafasi ya tatu, wakati wa Fainali za Kombe la Dunia za 2018 zilizofanyika nchini Urusi.