Mechi mbili za kwanza hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Azam (Azam Sports Federation Cup 2016/2017), zitachezwa Machi 18 na 19, mwaka huu kwenye viwanja viwili tofauti.
Mechi hizo ni kati ya Kagera Sugar itakayocheza na Mbao FC ya Mwanza kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba mkoani Kagera wakati siku inayofuata Machi 19 Simba itacheza na Madini kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Awali Simba ilikuwa icheze Machi 18, mwaka huu, lakini siku hiyo uwanja huo utakuwa na shughuli za kijamii hivyo sasa utachezwa siku ya Jumapili Machi 19, mwaka huu.
Mechi nyingine zitapangiwa tarehe za baadaye. Mechi hizo ni kati ya Azam FC na Ndanda FC kadhalika Tanzania Prisons ya Mbeya itakayocheza na mshindi kati ya Young Africans ya Dar es Salaam na Kiluvya United ya Pwani.
Bingwa wa michuano hiyo kwa mujibu wa kanuni, atazawadiwa Tsh. 50 milioni.
Pia bingwa wa michuano hiyo, ndiye atakayeiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ya Total wakati Bingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara ndiye ataiwakilisha nchi kwenye michuano ya Total Ligi ya Mabingwa Afrika.