Roma Mkatoliki amerejea kwenye taaluma yake ya awali ya ualimu na kuongeza nguvu ya ziada kwenye somo la hisabati, somo ambalo linaongoza kuwapiga mieleka wanafunzi katika ngazi zote za masomo nchini.
Mkali huyo ambaye amekuwa kimya kwenye muziki tangu lilipomfika tukio baya la kutekwa na kuteswa na watu wasiojulikana, leo alikuwa shule ya msingi Mchikichini jijini Dar es Salaam ambapo alitoa zawadi ya vitabu vya somo la hisabati kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Aidha, Rhymes of Magic Attraction (Roma), alitumia muda huo kama mwalimu na msanii ambaye ana nafasi ya kuwa kioo cha jamii, kuwatia moyo wanafunzi hao katika safari yao ya masomo.
Roma aliingia rasmi kwenye ulimwengu wa muziki na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwateka mashabiki akitokea jijini Tanga, ambapo wimbo wake wa ‘Hii ndio Tanzania’ uligeuka kuwa ‘wimbo wa taifa la vijana’.
Hivi karibuni mkali huyo alieleza kuwa baada ya tukio la kutekwa, anahitaji muda wa kutafakari na kurejea kisaikolojia ndipo afahamu kitakachofuata kwenye muziki wake.
“Unajua muziki ni hisia, siwezi kusema kuwa nikiingia studio nitafanya nini kwa sasa, inategemea ntakuwa na hisia gani wakati huo,” alisema Roma.
Huenda kukawa na mtihani wa kuanza kuandika upya baadhi ya nyimbo zilizokuwa kwenye hatua za utayarishaji kwani watekaji waliondoka na computer ya studio za Tongwe Reords iliyokuwa ikitumika kuandaa na kutunza nyimbo zake.