Nahodha na Mshambuliaji wa kikosi cha Ubelgiji, Romelu Lukaku amesema atamkaribisha Thibaut Courtois kurejea katika timu hiyo kwa mikono miwili baada ya mlinda mlango huyo kutangaza kustaafu kukichezea kikosi hicho Juni, mwaka huu.

Akiwa amevuliwa unahodha, Courtois alikataa kucheza mechi ya kufuzu michuano ya Ulaya dhidi ya Estonia iliyochezwa Juni, kwa mujibu wa Kocha, Domenico Tedesco ambaye juma hili alisema tangu wakati huo hajawasiliana na mlinda mlango huyo wa Real Madrid.

Courtois alipasuka mishipa ya goti na kufanyiwa upasuaji Agosti, na kumweka nje kwa muda wa miezi sita, lakini mapema juma hili beki wa pembeni wa Ubelgiji, Timothy Castagne alisema hafikirii Courtois anaweza kurejea kikosini bila maelezo yoyote.

Hata hivyo, Lukaku, alitoa maoni tofauti juu la Courtois kurejea kwenye kikosi hicho.

“Namaanisha kutoka moyoni mwangu, lazima tuweke kile kilichotokea nyuma yetu,” alisema Lukaku akiwaambia waandishi wa habari wakati Ubelgiji ikijiandaa kwa mechi ya kufuzu dhidi ya Austria itakayopigwa mjini Vienna leo.

“Siku Thibaut akiamua kurejea atarudi tu, ikitokea hivyo bado atakuwa wa thamani kubwa. Thibaut atajijibu mwenyewe kwenye chumba cha kubadilishia nguo.

“Tunahitaji kuyaweka sawa mambo hayo. Kupona kwaThibaut ndilo jambo muhimu zaidi sasa, na akirejea, nitakuwa wa kwanza kumkaribisha kwa mikono miwili.”

Lukaku alichaguliwa mbele ya Courtois kama nahodha Juni, akisimama badala ya Kevin De Bruyne ambaye ni majeruhi.

Robertinho akoshwa na kiwango cha Ngoma
Ally Mayay: Tanzania ipo tayari kwa AFL