Aliyekua meneja wa klabu ya Everton Ronald Koeman ameelezea masikitiko yake, baada ya kufungashiwa virago huko Goodson Park hapo jana, kufuatia hali kumuendea kombo katika utendaji wake wa kazi.

Koeman alionyeshwa mlango wa kutokea, baada ya kikosi chake kukubali kichapo cha mabao matano kwa mawili mbele ya Arsenal, katika mchezo wa mwishoni mwa juma lililopita, hali ambayo iliendelea kudhihirisha udhaifu wa kazi yake tangu msimu huu ulipoanza.

Meneja huyo kutoka nchini Uholanzi amesema haikua rahisi kukubaliana na hali ya kuondoka klabuni hapo, lakini ilimlazimu kuondoka kutokana na makubaliano yaliyofikiwa kati yake na viongozi wa Everton, ambao juzi walikasirishwa na kichapo kilichotolewa na Arsenal.

Koeman amesema aliishi vizuri na kila mmoja huko Goodinon Park na maisha yalikua safi, lakini mazingira ya uwnajani pindi kikosi chake kilipocheza hayakumpendeza yoyote anaeipenda klabu hiyo yenye maskani yake makuu mjini Liverpool.

Hata hivyo Koeman ambaye alijiunga na Everton akichukua nafasi ya Roberto Martinez mwanzoni mwa msimu uliopita akitokea Southampton, ameitakia kila la kheri The Toffees katika harakati za mapambano ya kushinda msimu huu na kufikia lengo linalokusudiwa.

“Ninapenda kumshukuru kila mmoja tuliyefanyanae kazi Goodison Park, tulikua na maisha mazuri wakati wote, lakini imebidi kuondoka kutokana na hali iliokuwa inanikabili,” amesema Koeman kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter.

“Ninamshukuru mwenyekiti Bill Kenwright, mwanahisa mkuu wa klabu Farhad Moshiri pamoja na bodi yote ya uongozi kwa nafasi waliyonipa ya kukiongoza kikosi cha klabu kubwa kama Everton, pia sitowasahau mashabiki, ambao siku zote walionionyesha ushirikiano wa kutosha.

“Kwa hakika nimesikitishwa sana na hatua hii, lakini sina budi kukubali na kumtakia kila la kheri yoyote mwenye mapenzi mema na klabu.”

Nafasi ya Koeman mwenye umri wa miaka 54, tayari imeshajazwa na aliyekua kocha wa kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 23 David Unsworth, ambaye atakuwa mkuu wa benchi la ufundi kwa muda, wakati uongozi ukiendelea kumsaka meneja mwingine.

Koeman anakua meneja watatu kutimuliwa katika ligi ya nchini England msimu huu, akitanguliwa na muholanzi mwenzake Frank De Boer aliyekua anakiongoza kikosi cha Crystal Palace, pamoja na Craig Shakespeare aliyekua mkuu wa benchi la ufundi la Leicester City.

Taa za uwanjani zaiponza Besiktas
Uchaguzi wa marudio wapingwa tena Kenya