Mshambuliaji wa mabingwa wa soka nchini Hispania Real Madrid, Cristiano Ronaldo ameadhibiwa kwa kufungiwa michezo mitano baada ya kubainika kuwa alimsukuma mwamuzi, Ricardo de Burgos Bengoetxea mara baada ya kuoneshwa kadi nyekundu katika mchezo wa ‘Spanish Supercup’ dhidi ya FC Barcelona uliochezwa usiku wa kuamkia leo.
Ronaldo alionyeshwa kadi nyekundu iliyoambatana na kadi ya pili ya njano, baada ya kujiangusha kwa makusudi ya kumuahadaa mwamuzi huyo, ambaye alichezesha mpambano wa mkondo wa kwanza wa Spanish Supercup uliomalizika kwa Real Madrid kuchomoza na ushindi wa mabao matatu kwa moja dhidi ya mahasimu wao.
Kwa kuonyesha hasira dhidi ya mwamuzi, Ronaldo alimsukuma mgogoni Bengoetxea, jambo ambalo lilimtia hatiani.
Kwa mujibu wa kifungu cha 96 cha kanuni za soka za Chama cha Soka cha Hispania kitendo cha kumsukuma mwamuzi kinaweza kumfanya mchezaji afungiwe mechi nne hadi 12.
Kwa mantiki hiyo Ronaldo atakosa mchezo wa mkondo wa pili wa Spanish Supercup utakaochezwa jumatano ya juma hili, sambamba na michezo mingine ya ligi.
Michezo ya ligi itakuwa kati ya Real Madrid dhidi ya Deportivo La Coruna, Valencia, Levante na Real Sociedad.