Mshambuliaji na nahodha wa timu ya taifa ya Ureno Cristiano Ronaldo amempiku mpinzani wake, Lionel Messi kwenye mchakato wa wanasoka waliovuna mkwanja mrefu zaidi kwa mwaka 2020 kama ilivyoelezwa kwenye orodha mpya ya jarida la Forbes.
Mjumuiko wa mishahara ya mshambuliaji huyo wa mabingwa wa Italia (juventus FC) na pesa nyingine anavuna kupitia soka lake la uwanjani pamoja na dili za matangazo umemshuhudia Ronaldo akiweka kibindoni Pauni 85.8 milioni kwa mwaka 2020, akiwa amezidiwa na staa wa tenisi, Roger Federer, ambaye anashika usukani kwa kuwa mwanamichezo aliyevuna pesa nyingi zaidi duniani.
Messi anashika namba tatu kwenye orodha yote, lakini ni namba mbili kwa wanasoka, kutokana na kuvuna Pauni 83.4 milioni, huku hilo likija baada ya Barcelona kuamua kump-unguzia mshahara wake kutokana na janga la corona.
Anayefuatia kwenye orodha ni Mbrazili, Neymar ambaye amevuna Pauni 76.6 milioni, huku staa huyo wa Paris Saint-Germain, akivuna Pauni 20 milioni kutoka kwenye dili zake za matangazo.
Mshambuliaji wa Liverpool, Mohamed Salah anafuatia kwenye orodha hiyo, lakini akishika namba moja kwa upande wa Ligi Kuu England baada ya kuvuna Pauni 28.2 milioni ndani ya mwaka huu na kumpiku kinda wa PSG na timu ya taifa ya Ufaransa, Kylian Mbappe.
Mbappe amevuna Pauni 27.1 milioni ndani ya mwaka huu, huku orodha hiyo ikiwahusu pia mastaa Andres Iniesta, anayekipiga Vissel Kobe ya Japan, kiungo wa Arsenal, Mesut Ozil, staa wa Manchester United, Paul Pogba, kiungo wa Shanghai SIPG, Oscar na mkali wa Barcelona, Antoine Griezmann.