Aliyekua mshambuliaji mahiri wa timu ya taifa ya Brazil Ronaldo Luís Nazário de Lima ameripotiwa kuwa kwenye mipango ya kuinunua klabu ya Real Valladolid iliyopanda daraja na kucheza ligi kuu ya Hispania (La Liga) msimu huu wa 2018/19.
Ronaldo mwenye umri wa miaka 41, endapo atakamilisha mpango wa kuinunua klabu hiyo yenye maskani yake makuu José Zorrilla, Valladolid, atakuwa rais wa klabu hiyo.
Tayari mazungumzo kati ya gwiji huyo wa soka duniani na mmiliki wa sasa wa klabu hiyo Carlos Suarez yameshaanza, na imeriportiwa Ronaldo yupo tayari kutoa kiasi cha Euro milioni 30 ambazo ni sawa na Pauni milioni 27.2.
Hata hivyo Ronaldo anakabiliwa na upinzani kutoka kwa mfanyabiashara wa Mexico Ernesto Tinajero ambaye ameonyesha kuwa tayari kuinunua klabu hiyo.
Mfanyabiashara huyo aliwahi kuwa kiongozi wa Real Valladolid, lakini mahusiano yake na viongozi wengine klabuni hapo kama Jose Moro (Rais wa zamani) na Jose Luis Losada (makamu wa Rais) yalivunjika, na akaamua kujiuzulu.
Endapo Ronaldo atafanikisha mpango wa kuinunua klabu hiyo na kuimiliki, atakua amerejea rasmi katika medani ya soka la Hispania, ambapo aliwahi kuwa mchezaji kwa muda wa misimu sita akiwa na Rel Madrid.