Mshambuliaji na nahodha wa timu ya taifa ya Ureno Cristiano Ronaldo dos Santos Aveiro, ameweka rekodi mpya katika maisha yake ya soka, baada ya kuifungia klabu yake ya Juventus FC katika dakika ya 57, kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya dhidi ya Dynamo Kiev, usiku wa kuamkia leo.

Juventus FC waliibuka na ushindi wa mabao matatu kwa sifuri kwenye mchezo huo, Ronaldo akifunga bao moja miongoni mwa mabao hayo ambayo yameipelekea klabu hiyo kwenye hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya.

Hatua ya kufunga bao hilo limemfanya mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 35, kufikisha magoli 750 tangu alipoanza kucheza soka la kiushindani mwaka 2002 akiwa na klabu ya Sporting CP kikosi B.

Ronaldo ambaye ni mshindi mara 5 wa tuzo ya Ballon d’Or, alipokuwa Real Madrid alifunga mabao 450 katika michezo 438, na wakati akiwa Manchester United, alifunga jumla ya magoli 118, huku bao la usiku wa kuamkia leo dhidi ya Dynamo Kiev, ni bao lake la 75 akiwa na Juventus.

Baada ya kuweka rekodi hiyo, Cristiano Ronaldo aliwashukuru wachezaji wenzake, kocha na wapinzani wake kwa kuwa na mchango katika kufikia hatua hiyo.

Ronaldo alisema:  “Mabao 750, nyakati za furaha 750, nyuso 750 za furaha kwa mashabiki wetu. Ninawashukuru wachezaji na makocha wote ambao wamenisaidia kuifikia hii namba, ninawashukuru wapinzani wangu wote kwa kunifanya niongeze juhudi katika utendaji kazi wangu.”

Ronaldo atakua na safari nyingine ya kuendeleza rekodi ya kutafuta bao la 751  mwishoni mwa juma hili kwenye mchezo wa Ligi ya Italia dhidi ya Torino mwishoni mwa juma hili. Katika michezo minne dhidi ya Torino, Ronaldo amefunga kwenye mechi 3.

UN yaiondoa bangi kwenye orodha ya madawa hatari ya kulevya
Unyanyasaji wa kijinsia umehamia mitandaoni

Comments

comments