Mwanasheria wa Saudi Arabia ametoa wito wa kufukuzwa mchezaji wa Al Nassr Cristiano Ronaldo kufuatia kitendo kinachodaiwa kuwa si cha kimaadili katika nchi hiyo ya Kiislamu.
Nyota huyo wa zamani wa Manchester United alikuwa akiichezea Al Nassr dhidi ya Al Hilal siku ya Jumanne wakati tukio hilo linalodaiwa kutokea.
Ronaldo alicheza dakika zote 90 katika kichapo cha mabao 2-0, lakini baadaye alizomewa na mashabiki muda wote.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 38 alionekana kushika sehemu zake za siri alipokuwa akitoka nje ya uwanja, huku wafuasi wakiimba jina la Lionel Messi ndani ya Uwanja wa Kimataifa wa King Fahd mjini Riyadh.
Ikiwa kwa makusudi, tabia ya Ronaldo inachukuliwa kuwa haramu nchini Saudi Arabia.
Baada ya video hiyo kuonekana kwenye mitandao ya kijamii, wakili Nouf bin Ahmed alisema aliwasilisha malalamiko katika Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Saudi Arabia, na kuongeza Ronaldo anatuhumiwa kufanya ‘kosa la uchafu’.
“Inachukuliwa kuwa ni uhalifu wa kuvunjia heshima umma, na ni moja ya uhalifu unaohusisha kukamatwa na kufukuzwa nchini ikiwa itafanywa na mgeni,” alisema wakili huyo aliyebobea katika Sheria za Kimataifa.”
Taarifa ya klabu ilisema kwamba “Ronaldo anauguza jeraha na changamoto yake ya Gustavo Cuellar, mchezaji wa Al-Hilal, ilianza kwa pigo katika eneo nyeti sana. Hii ni habari iliyothibitishwa. Kuhusu maelezo ya mashabiki, wako huru kufikiria chochote wanachotaka.”
Ronaldo, ambaye ameichezea timu ya taifa ya Ureno mara 198, ameifungia Al Nassr mabao 11 katika mechi 11 za ligi hadi sasa msimu huu.