Mshambuliaji na nahodha wa timu ya taifa ya England Wayne Mark Rooney usiku wa kuamkia hii leo aliweka rekodi ya kuwa kinara wa kupachika mabao kwenye timu ya taifa ya nchi hiyo.

Rooney alifunga bao la pili kwa mkwaju wa penati dhidi ya Uswiz katika mchezo wa kuwania kucheza fainali za mataifa ya barani Ulaya baada ya mshambuliaji wa Spurs, Harry Kane kufunga bao la kwanza.

Rooney amefikisha mabao 50 katika michezo 107 aliyocheza akiwa na timu ya taifa ya England ambayo alianza kuitumikia 2003.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 29, alionyesha dhamira ya kujiweka kwenye kilele cha ufungaji bora katika orodha ya wachezaji wa timu ya taifa ya England kwa wakati wote, baada ya kufunga moja ya mabao kati ya mabao sita yaliyoipa ushindi timu hiyo wakati wa mchezo dhidi ya San Marino uliochezwa mwishoni mwa juma lililopita.

Katika orodha ya wafungaji bora ya timu ya taifa ya England, mkongwe Bobby Charlton aliyeichezea timu hiyo kuanzia mwaka 1958–1970 alikua akiongoza kwa kufunga mabao 49 ambayo aliyapata kwenye michezo 106 aliyocheza.

Ushindi wa mabao amwili kwa sifuri dhidi ya Uswiz uliopatikana usiku wa kuamkia hii leo, umeendelea kuiweka kileleni kwa mapana na marefu timu ya taifa ya England katika msimamo wa kundi la tano kwa kufikisha point 24, huku tayari ikiwa imeshapata tiketi ya kwenda nchini Ufaransa zitakapofanyika fainali za barani Ulaya mwaka 2016.

Serena Williams Amtesa Tena Ndugu Yake
Austria Yakata Tiketi Ya Kucheza Euro 2016