Mfanya maarufu nchini Tanzania, Rostam Azizi, na mbunge wa Ubungo, Prof. Kitila Mkumbo, wamemshukia vikali Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, kwa kutoa kauli za ubaguzi dhidi ya Wazanzibari kwenye mjadala unaoendelea wa uwekezaji binafsi katika bandari ya Dar es Salaam na kumshangaa mwanasiasa huyo kwa kuleta siasa za ukaburu kwenye jambo la kiuchumi na kibiashara.
Bila kumtaja Mbowe kwa jina, Rostam na Kitila wameonesha kukerwa na kushtushwa na kauli za kibaguzi ambazo Mbowe amezitoa dhidi ya Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof Makame Mbarawa, kwa kuhusisha asili yao ya Zanzibar na maamuzi ya uendeshaji wa bandari ya Dar es Salaam.
Kauli hizo za kibaguzi za Mbowe, ambazo zimerudiwa na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu na aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Wilibrod Slaa, zimechochea mjadala wa kibaguzi wa wanaojiita Watanganyika dhidi ya Wazanzibari kwenye suala la bandari ya Dar es Salaam.
“Hizi siku za karibuni nimekuwa nasikiliza huu mjadala kuhusu uendeshaji wa bandari (ya Dar es Salaam). Sina tatizo na watu kukosoa vitu. Lakini kilichonitatanisha, kunisikitisha na kunisononesha na kunitisha ni sura ya mjadala wenyewe. Ukachukua sura ya kisiasa ya ushabiki na hata hao viongozi walioamua kutumia siasa katika hili jambo wakahusisha na dini,” Rostam alisema kwenye mdahalo wa kitaifa uliofanyika Dar es Salaam leo.
“Ni bahati mbaya sana kwamba mjadala wa kiuchumi na kibiashara unageuzwa kuwa mjadala wa kisiasa, wa kishabiki na wa kidini. Hili jambo halina afya kwa nchi yetu.”
Rostam alikuwa ni miongoni mwa watoa mada kwenye mdahalo huo ulioandaliwa na kampuni ya Media Brains jijini Dar es Salaam.
Bila kutaja jina la mwanasiasa yoyote yule, Rostam alikemea uchochezi wa kidini na nyufa za muungano unaochochewa na wanasiasa wakubwa wa vyama vya upinzani nchini.
“Unamuona kiongozi mkubwa kabisa anaanza kuzungumza habari ya Uzanzibari na Utanganyika kwenye suala la kibiashara na kiuchumi. Ni hatari kwa nchi yetu, ni hatari kwa umoja wetu,” Rostam alisema.
Rostam alionya kuwa umoja wa kitaifa ambao umeasisiwa na Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume sasa umeanza kupata ufa kutokana na kauli za kibaguzi za viongozi wakubwa wa siasa.
“Leo hii tunaposema mtu ni Mzanzibari ndiyo maana amefanya maamuzi haya, kesho tutasema huyu Rais ametoka Mbeya, hana haki ya kufanya maamuzi kwa mgodi wa Mara,” Rostam alionya.
Naye Kitila alisisitiza kuwa ni muhimu kwa viongozi wa kisiasa kuheshimu dhamana yao ya kitaifa bila kujali kama wako kwenye chama tawala au vyama vya upinzani.
“Nchi yetu ina pande mbili za muungano. Hatuwezi kumhukumu mtu kwa sababu ametoka pande moja ya muungano. Kama kiongozi amekosea, asihukumiwe kwa sababu anatoka wapi. Ukifanya hivyo, unaacha dhamana ya kiongozi unakwenda kugusa mambo ya msingi yanayofanya taifa letu kuwa taifa,” alisema.
Kitila alimshauri Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Godbless Lema, ambaye alihudhuria mjadala huo kuangalia na chama chake namna ambavyo Mbowe anaweza kuwaomba radhi Watanzania kwa kauli zake za kibaguzi dhidi ya Wazanzibari na kuzifuta kauli hizo.
“Mimi nadhani katika hali ya kistaarabu nyie (CHADEMA) mkikaa kwenye uongozi, Mwenyekiti wetu wa taifa (Freeman Mbowe) anaweza akatafuta namna ya ku-apologise (kuomba radhi) na ku-withdraw statement zake (kufuta kauli). Kwa sababu anaposema kwa nini bandari za Zanzibar hazijahusishwa, sisi tumefanya mambo mengi bara kwa nini hatukuuliza hatukujenga Zanzibar,” alisema.
“Waongee wengine huko kwenye vijiwe, lakini sisi kama viongozi wa kitaifa lazima tuchukue dhamana. Inawezekana mwenyekiti wetu (Mbowe) alipata jazba aka apologise (akaomba radhi).”