Aliyekua kocha mkuu wa timu ya taifa ya England Roy Hodgson anatajwa kuwa katika mazingira mazuri ya kukabidhiwa jukumu la kuwa mkuu wa benchi la ufundi la klabu ya Leicester City.
Hodgson ambaye alikiongoza kikosi cha England wakati wa fainali za kombe la dunia za mwaka 2014 na kisha fainali za Ulaya (Euro 2016), ni miongoni mwa walioorodheshwa kuchukua nafasi ya Claudio Ranieri tangu alipotimuliwa mwishoni mwa juma lililopita.
Jina la babu huyo mwenye umri wa miaka 69, limechukua nafasi kubwa katika vikao vya bodi ya Leicester City, ambayo tangu mwishoni mwa juma lililopita imekua na vikao vya mara kwa mara kwa ajili ya kujadili ajira ya meneja mpya.
Kwa mujibu wa gazeti la The Sun la nchini England, Hodgson huenda akatajwa kuwa meneja wa Leicester City baada ya mchezo wa ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya Sevilla utakaochezwa majuma majuma mawili yajayo.
Kwa sasa viongozi wa juu wa Leicester City wataendelea kumuamini meneja wa muda Craig Shakespeare ambaye alikiongoza kikosi cha The Foxes kupata ushindi wa mabao matatu kwa moja dhidi ya Liverpool usiku wa kuamkia jana.
Mbali na kukinoa kikosi cha timu ya taifa ya England, Hodgson aliwahi kuvinoa vikosi vya klabu za West Brom, Fulham na Liverpool.
Kwa mara ya mwisho Hodgson alifanya kazi yake ya ukufunzi wa soka katika mchezo wa Euro 2016 hatua ya 16 bora, ambapo England ilishindwa kufurukuta mbele ya Iceland kwa kufungwa mabao mawili kwa moja.