Aliyekua kocha mkuu wa timu ya taifa ya England Roy Hodgson ametangawa rasmi kuwa meneja wa kikosi cha klabu ya Crystal Palace inayoshiriki ligi ya EPL.
Hodgson alitangazwa kushika nafasi hiyo usiku wa kuamkia leo, kufuatia kutimuliwa kwa mholanzi Frank de Boer siku ya jumatatu, baada ya kushindwa kufikia lengo la kuisaidia Crystal Palace katika michezo ya awali ya ligi ya England.
Kazi yake ya kwanza akiwa na Crystal Palace itakua mwishoni mwa juma hili ambapo atakua mwenyeji wa Southampton, kisha atacheza dhidi ya Manchester City na Manchester United ugenini, kabla ya kuwakabili mabingwa watetezi Chelsea kwenye uwanja wake wa nyumbani.
“Natumai kufanya kazi yangu kwa umakini mkubwa, kutokana na uzoefu nilionao, imekua kama bahati kwangu kurejea tena katika tasnia ya ukufunzi wa soka, baada ya kukaa pembeni tangu mwaka 2016 nilipojiuzulu kuifundisha timu ya taifa,” Alisema Hodgson baada ya kukamilisha mpango wa kujiunga na klabu hiyo ya jijinji London.
“Ni siku nzuri kwangu ambayo itaendelea kubaki katika kumbukumbu za maisha yangu, ninajivunia kuwa sehemu ya walioheshimiwa ndani ya klabu hii, sina budi kuangalia mbele katika majukumu ya kazi yangu ambayo inaanza mara moja, ili kuirudisha Crystal Palace katika hadhi yake ya kushindana.” Aliongeza Hodgson.
Kwa mara ya mwisho Hodgson alionekana katika benchi la ufundi wakati wa mchezo wa Euro 2016 dhidi ya Iceland walioibuka na ushindi wa mabao mawili kwa moja mwezi Juni 2016.
Kwa upande wa ligi ya England, kwa mara ya mwisho alikinoa kikosi cha West Bromwich Albion, kabla ya kutangazwa kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya England mwaka 2012. Pia aliwahi kuvifundisha vikosi vya Blackburn Rovers, Fulham na Liverpool.