Nahodha na Kiungo wa zamani wa Manchester United Roy Keane amesema haamini kama Arsenal wanaweza kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu ya England msimu huu 2022/23, na badala yake ameipa nafasi kubwa Manchester City kutetea taji lake.
Akizungumza kwenye kipindi cha ‘The Overlap’ kinachoendeshwa na mchezaji mwenzake wa zamani wa Man Utd Gary Neville, Keane ambaye ni mchambuzi raia wa Ireland amedai Arsenal itaendelea kupata ushindi katika michezo ya karibuni, lakini itakwama itakapokutana na Man City, na kupoteza mwelekeo wa Ubingwa.
Keane amesema vijana wa Pep Guardiola ndio mabingwa watetezi na wameshinda michuano minne kati ya mitano iliyopita, hivyo wana ari kubwa ya kupambana na wanajua utamu wa kushinda taji hilo kwa mata ya pili mfululizo msimu huu.
City wapo nyuma kwa mchezo mmoja dhidi ya The Gunners, hii inamaanisha kama watashinda kiporo chao basi watakuwa nyuma kwa alama tano pekee. Hadi sasa City ikiwa imebakiwa na michezo 10 pekee msimu huu na Arsenal ina michezo tisa.
Gwiji huyo wa Manchester United alikiri kwamba wachezaji wa Mikel Arteta wanapewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa lakini kwa upande wake yuko tofauti.
Amesema: “Wao (Arsenal) wapo kwenye nafasi nzuri, wasingefikiria hilo. mwanzoni mwa msimu lakini wamekuwa na kipaji, wachezaji wengi vijana wamekuwa na msimamo, wanaweza kuzingatia tu ligi.
“Bila shaka ni wachezaji wazuri. Sidhani kama watafanya hivyo hadi mwisho, bado natakiwa kuipenda City lakini Arsenal wamejiweka katika nafasi nzuri.”
“Unahitaji bahati kidogo, majeraha katika miezi michache iliyopita, wako katika nafasi nzuri na lazima uwavutie kwa hilo hauwezi kuwachukia.”
“Ila nadhani City ni wazuri sana, mechi ambazo (Arsenal) wanapaswa kwenda na kushinda zimekuwa na shinikizo na hawajashughulikia hilo kwa miaka michache iliyopita.”
Miongoni mwa michezo iliyosalia ambayo itaikabili Arsenal ni dhidi ya Liverpool, Chelsea na Newcastle, pamoja na pambano linaloweza kubainisha ishu ya ubingwa kwenye Uwanja wa Etihad wa City Aprili 26.
Hata hivyo, Arsenal kwa sasa wanapambana zaidi kwenye ligi baada ya kuondolewa kwa Europa, wakati City bado wako kwenye Ligi ya Mabingwa na Kombe la FA.
Kituo kinachofuata, kikosi hicho cha Kaskazini mwa London kitasafiri hadi Anfield kumenyana na Liverpool keshokutwa Jumapili (April 09).