Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro leo Machi 29, 2022 amefanya uhamisho na mabadiliko kwa baadhi ya makamanda wa polisi wa mikoa.
Katika uhamisho huo, aliyekuwa RPC Mkoa wa Kagera, ACP Wankyo Nyigesa amehamishiwa Makao Makuu ya Polisi Dodoma na nafasi yake inachukuliwa na aliyekuwa RPC Rukwa, ACP William Mwampagale.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, uhamisho huo umefanyika ili kupisha uchunguzi wa tukio la tarehe 26.3.2022 katika sherehe ya kumuaga ACP Wankyo ambapo alitoa maneno ambayo yanaonyesha kuwepo na ukiukwaji wa nidhamu kulingana na miongozo ya Jeshi la Polisi.
Wakati akiwa kamanda wa Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Pwani (ACP) Wankyo Nyigesa aliwahi kutoa jumbe zinazoonesha kutishiwa na watu wasiofahamika kupitia ujumbe mfupi wa simu (SMS) kuwa watamhamisha kwenye mkoa huo kutokana na kuzuia kuingiza bidhaa za magendo kwenye bandari bubu.
“Sitishwi na mtu wala sms eti watatuhamisha ama watatupeleka Mlingotini waambieni meseji zao tunazo, tunazifanyia kazi na tumechukua namba za hawa tuliowakamata kutokana na operesheni hizi kama ni miongoni mwao tutawachukulia hatua kali,“alieleza Nyigesa.
Pia katika mabadiliko hayo, aliyekuwa Afisa Mnadhimu Mkoa wa Rukwa, ACP Theopista Mallya anakuwa RPC wa mkoani Rukwa aliyekuwa Mkuu wa Operesheni Rukwa, ACP Mashenene Mayila anakuwa Afisa Mnadhimu wa mkoa huo