Sakata la kuwepo watuhumiwa wanaowalawiti watoto jijini Dar es Salaam limeibua sintofahamu baada ya wakaazi wa Wilaya ya Temeke jijini humo kupinga dhamana aliyopewa mtuhumiwa anayefahamika kwa jina maarufu la ‘Nguruwe’.
Kutokana na sintofahamu hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Amon Kakwale alishiriki katika kipindi cha On The Bench cha Dar24 Media, ambapo alijadiliana moja kwa moja na wananchi wa Kata ya Sandali akiwa na maafisa kutoka Dawati la Jinsia na Watoto la Jeshi hilo.
Akizungumza baada ya kuwasikiliza wananchi walioongozwa na Mwenyekiti wa mtaa wa Vetenari, Ali Mwamba, RPC Kakwale alisema kuwa imekuwa fursa nzuri kwake kuwasikiliza wananchi wakizungumza moja kwa moja na kuyatafutia ufumbuzi wa haraka matatizo waliyoyaibua.
“Nichukue fursa hii kwanza kuwashukuru wananchi wote wa Mtaa wa Mamboleo, Kata ya Sandali kwa kufika kwenu, lakini kubwa kwa kusema kwa uwazi yale ambayo mwaamini yanaweza kuwa chanzo au chimbuko la matukio haya ya kulawiti,” alisema RPC Amon Kakwale.
“Mimi kwenu, kama ambavyo nawasikia mnavyochangia nafarijika sana kwa sababu nasikia kutoka kwenu moja kwa moja tofauti na pale ambapo naweza kuletewa labda na mkuu wa kituo au na mkuu wa upelelezi lakini leo napata ‘live’ kutoka kwenu,” aliongeza.
RPC Kakwale alitoa rai kwa wananchi kutojichukulia hatua mikononi na badala yake waripoti katika kituo cha polisi na kuacha sheria ichukue mkondo wake.
Aidha, baada ya wananchi hao kumsihi RPC kumrejesha mahabusu mtuhumiwa wa vitendo vya ulawiti ingawa alikuwa amepewa dhamana. Kamanda huyo wa polisi aliridhia akieleza kuwa anaondoka naye kwa ajili ya usalama wake.
On The Bench ni kipindi kinachowakutanisha wananchi na wataalam, viongozi mbalimbali ili kujadili na kutafuta ufumbuzi wa changamoto na matatizo yanayowasibu.