Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga, limesema kuwa tukio la wenye silaha za moto wanaosadikika kuwa ni majambazi waliovamia ‘Hostel’ za wanafunzi wa Chuo Cha Kumbukumbu ya Sebastian Kolowa (Sekomu), lilitekelezwa kwa lengo la kuwatia wananchi hofu ya ugaidi.

Akizungumza na Dar24 kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, SACP Benedict Wakulyamba alisema kuwa wahalifu hao walitaka kuwatia hofu wananchi kama inavyoonekana hivi sasa ambapo wanafunzi wa eneo hilo wamekumbwa na hofu kufuatia tukio hilo.

Aidha, Kamanda Wakulyamba alisema kuwa tukio hilo halina uhusiano wowote na ugaidi na kwamba hakuna tukio lolote la kigaidi lililotekelezwa nchini hivi karibuni, bali matukio mengi yamekuwa yakifanywa na makundi ya wahalifu ambao sio magaidi.

“Kama nilivyosema kuwa lengo lao ni kutia hofu, na kama unavyoona sasa wanafunzi ni kama wamekumbwa na hofu,” Kamanda Wakulyamba aliiambia Dar24.

Alisema kuwa hakuna tukio lolote la kigaidi lililotekelezwa na kikundi chochote cha kigaidi hapa nchini hivi karibuni, bali kinachofanywa ni vitisho vya watu waliolenga katika kuwatia wananchi hofu.

“Hii ni ishara ya wazi kwamba hawa watu wanafanya hivi vitendo kwa lengo la kutishia watu . lakini sisi kama mkoa wa Tanga hatuwezi kusema kama wale ni magaidi kwa sababu mbili… tunaendelea kufanya uchunguzi kubaini ni vikundi vya aina gani. Lakini pili,hakuna kikundi chochote cha kigaidi kilichojitangaza kuhusika na tukio hilo kwani ndio tabia yake,” alisema Kamanda huyo wa Polisi Mkoa Tanga.

Alisema kuwa baada ya tukio hilo, Jeshi hilo limelichukua kama sehemu ya viashiria vya kigaidi na itavifanyia kazi.

“Jeshi la Polisi liko imara, linaendelea kufanya uchunguzi wa tukio hilo. Nina amini kwamba wahusika wote wa tukio hilo tutawakamata na watawajibishwa kwa mujibu wa sheria,” tunamkariri.

Juzi usiku, watu wanaosadika kuwa ni majambazi walivamia chuo cha Sekumu na kumuua mlinzi mmoja kabla ya kujaribu kuchoma baadhi ya mabweni kwa kumwaga mafuta aina ya petrol.

Mwakyembe; Serikali Imeimarisha Mahakama Zote Nchini Kuwashughulikia Wahalifu
Rais Magufuli Atembelea Makaburi Ya Marais Watangulizi Wa Zanzibar Na Kusoma Dua Ya Pamoja