Kamanda wa Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam, Camillius Wambura amesema miongoni mwa sababu za kuibuka kwa wimbi la ujambazi katika Mkoa wa Dar es Salaam ni uwepo wa waliokuwa wafungwa waliopata msamaha hivi karibuni.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 28, 2021 jijini Dar es Salaam Kamanda Wambura amesema ni kawaida kuongezeka kwa matukio ya uhalifu mtaani wakati wafungwa wanapoachiwa huru na kurudi uraiani kwani wengi wanakuwa hawajaacha tabia za uhalifu zilisababisha wao kufungwa.

Aidha, Jeshi la Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam limemua jambazi mmoja aliyekutwa na silaha aina ya short gun jana Mei 27, 2021 katika fukwe za bahari ya Hindi eneo la Msasani.

Kamanda Wambura ameeleza kuwa chanzo cha tukio hilo ni kukamatwa kwa jambazi aliyefahamika kwa jina la Kilambo Nyasahiro maeneo ya Chanika kufuatia ufuatiliaji uliotokana na matukio ya ujambazi aliyoyafanya jijini Dar es Salaam na Mkoani Mara, Wilaya ya Tarime ambapo pia amekuwa akijihusisha na matukio ya ujambazi kwa muda mrefu.

“Baada ya kukamatwa na kuhojiwa aliweza kuelezea ni wapi alipoficha bunduki ambayo anaitumia yeye pamoja na wenzake, hivyo alifikisha askari katika eneo la Msasani, kwenye fukwe ya bahari ambapo alikuwa amefukia silaha hiyo,” amesema Kamanda Wambura.

“Na katika uchimbaji silaha hiyo ilionekana lakini bahati mbaya jambazi huyu kwa kudhani kwamba askari wanapenda zaidi silaha kuliko yeye alikurupuka na kukimbia kuelekea baharini ndipo askari walimshtua kwa risasi hewani hakusimama na baadaye alipigwa risasi mguuni na nyingine kiunoni na ndizo zilisababisha kuvuja damu nyingi na kufariki,” ameeleza Kamanda Wambura.

Mbali na tukio hilo, Jeshi hilo linawashikilia watuhumiwa 25 kwa tuhuma mbalimbali.

Mgambo wanne matatani kwa tuhuma za mauaji
SADC yaunda jeshi la dharura kupambana na ugaidi