Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Ramadhan Kingai amekana kumtesa mshitakiwa Adam Kusekwa wakati wa kuandika maelezo yake ya onyo kama upande wa utetezi unavyodai.
Ameeleza hayo leo Septemba 15,2021 katika Mahakama Kuu Kitengo cha Makosa ya Uhujumu Uchumi mbele ya Jaji Mustafa Siyani, wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo ndogo kufuatia mapingamizi ya upande wa utetezi wakipinga kupokelewa kwa maelezo ya onyo ya mshitakiwa huyo.
Kingai ambaye ni shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka katika kesi ndogo ndani ya kesi ya Msingi ambaye pia ni shahidi wa kwanza katika kesi ya ugaidi dhidi ya Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe na wenzake .
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Robert Kidando Kingai amedai mshtakiwa Kusekwa hakuteswa na wala hawakuwa na haja ya kufanya hivyo kwani hata wakati wa ukamatwaji Polisi hawakutumia nguvu.
Pia Kingai amedai wakati wa kuwakamata washtakiwa walidhani kungeweza kutokea mazingira magumu kwa kwa kuwa walikuwa ni askari lakini hali ilikuwa tofauti na hakukuwa na shida yoyote.
Akijibu maswali ya Wakili wa utetezi Pater Kibatala kama kuna mahali popote ambapo alionesha washtakiwa katika kipindi chote walichokamatwa hadi kuwahoji kama walipewa chakula jambo ambalo Kamanda Kingai amedai hakuna mahali aliposema washtakiwa walipewa chakula kwa kipindi chote hicho.
Pia Wakili Kibatala alimuuza shahidi kama mshtakiwa Kusekwa aliwahi kumweleza kama anamatatizo ya afya yanayoshabihiana na ugonjwa wa akili (Stress) ,Kamanda Kingai amedai mshatakiwa aliwahi kumueleza ila hakufuatilia.
Aidha, Kibatala amemuuliza Kingai kuwa ni kwa sababu gani jalada la kesi dhidi ya washtakiwa lilifunguliwa Dar es Salaama na maelezo ya mashahidi wawili walioshuhudia upekuzi wa maungoni wakati wa kukamatwa kwa washtakiwa eneo la Rau Madukani Moshi yalichukuliwa kituo cha polisi cha kati Moshi.
Shahidi amedai kuwa walifanya hivyo kwa kuwa maelezo ya mashahidi yanaweza kuchukuliwa mahali popote na hata wangeweza kuandika palepale Rau madukani lakini hali ya pale ilikuwa hairuhusu.
Kufuatia hali hiyo shauri limeahirishwa hadi kesho ambapo itaendelea kwa upande wa Jamuhuri kumuhoji shahidi (Re examination)
Katika kesi hiyo ndogo ndani ya kesi ya msingi jumla ya mashaidi saba wanatarajiwa kutoa ushahidi kwa upande wa Jamuhuri.Mbali na Mshtakiwa Adam Kusewa, washtakiwa wengine ni Mohamed Lingwenywa, Hassan Bwire Hassan na Freeman Mbowe.