Imeripotiwa kuwa Kocha Mkuu wa RS Berkane, Florent Ibenge amepewa jukumu zito la kuifunga Simba SC Jumapili (Machi 13) katika mchezo wa Mzunguuko wa nne wa ‘Kundi D’ Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

RS Berkane ya Morocco itacheza dhidi ya Simba SC katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 2-0, walioupata mjini Berkane Jumapili (Februari 27).

Taarifa kutoka nchini Morocco zinaeleza kuwa, Uongozi wa klabu hiyo umemtaka Kocha Ibenge kushinda mchezo dhidi ya Simba SC ili kuokoa kibarua chake ambacho kipo shakani katika kipindi hiki.

Agizo hilo limekuja baada ya Kikosi cha RS Berkane kupoteza mchezo wa Ligi Kuu ya Morocco kwa mabao 2-0 dhidi ya Raja Casablanca siku ya Jumamosi (Machi 06).

Hata hivyo haitakua rahisi kwa kocha huyo kutoka DR Congo kufanikisha jukumu hilo, kutokana na hitaji la ushindi kwa Simba SC ambayo imejizatiti kutorudia makosa ya kupoteza mchezo kwa mara ya pili mfululizo kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Simba SC imekua na rekodi nzuri kwenye michuano ya kimataifa, inapokua Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, na mara ya mwisho ilipocheza uwanjani hapo iliibanjua ASEC Mimosas ya Ivory Coast mabao 3-1.

RS Berkane ndio kinara wa Msimamo wa ‘Kundi D’ ikiwa na alama 06, ikifuatiwa na Simba SC ya Tanzania yenye alama 04 sawa na USGN ya Niger huku ASEC Mimosas ya Ivory Coast ikiburuza mkia kwa kuwa na alama 03.

Pablo: Simba SC ina nafasi ya kutwaa ubingwa
Wachezaji Geita Gold FC wapongezwa