Klabu ya RS Berkane ya Morocco imewasilisha malalamiko kwenye Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) kuhusu mwamuzi kutoka DR Congo, Jacques Ndala Chuma alichezesha mchezo wa Mzunguuko wanne wa ‘Kundi D’ Kombe la Shiriskiho Barani dhidi ya Simba SC.

RS Berkane wamewasilisha malalamiko hayo, baada ya kutokuridhishwa na kiwango cha uchezeshaji wa mwamuzi huyo, hivyo wanaamini walifanyiwa kusudi ili wapoteza mchezo wakiwa ugenini.

Taarifa kutoka kwa maafisa wa RS Berkane imedai kuwa Ndala alihongwa ndio maana aliwanyima penati kwenye mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam, Jana Jumapili (Machi 13).

Taarifa hiyo imeongeza kuwa walipata bao la wazi lakini mwamuzi huyo alilikataa kwa kisingizo cha mchezaji wao alikuwa tayari ameshaotea (offside).

Katika hatua nyingine wamedai kuwa Simba SC ilikua inapoteza muda makusudi, lakini bado mwamuzi aliongeza dakika chache, hali ambayo wanaamini ni dhahir walinyongwa kwa makusudi ili wapoteze ugenini.

Klabu hiyo imelitaka Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ kumuadhibu mwamuzi Ndala na wasaidizi wake wote kwa kufungiwa kama itawezekana, kwa kushindwa kutenda haki katika mchezo huo uliomalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Bao pekee na la ushindi katika mchezo huo ulioshuhudiwa na Mashabiki 35,0000 lilipachikwa wavuni na Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Senegal Pappe Ousman Sakho na kuifanya Simba SC kufikisha alama 07 kwenye msimamo wa Kundi D.

Nafasi ya Pili kwenye msimamo wa kundi hilo inashikwa na ASEC Mimosas ya Ivory Coast yenye alama 06 baada ya kuifumua USGN mabao 2-1, sawa na RS Berkane inayoshika nafasi ya tatu, huku USGN ikishika nafasi ya 04 kwa kumiliki alama 04.

Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa kundi D itaendelea tena mwishoni mwa juma hili (Machi 20), ambapo Simba SC itakua ugenini ikicheza dhidi ya ASEC Mimosas nchini Benin, huku USGN ikiikaribisha RS Berkane mjini Niamey-Niger.

Basi la kampuni ya kilimanjaro lapata ajali
Wananchi wa Ngorongoro wapata makazi mapya