Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha imepanga kuanza kusikiliza rufaa iliyofunguliwa na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili Februari 14, 2022.
Hayo yamesemwa na Naibu Msajili Ruth Massam leo Desemba 13, 2021 ambapo amesema kuwa rufaa hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa na kupangiwa tarehe ya kuanza kusikiliza.
“Leo imekuja kwa ajili ya kupanga tarehe ya kuanza kusikilizwa. Itaanza kusikilizwa Februari 14, 2022 mbele ya Jaji atakayepangiwa na itaendelea mfulululizo kama mtakavyoelekezwa,”amesema
Rufaa hiyo namba 129 ya mwaka huu, wajibu Rufaa (Jamhuri), waliwakilishwa na jopo la mawakili wanne wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu Tumaini Kweka, Mawakili wa Serikali Waandamizi Ofmed Mtenga, Felix Kwetukia na Wakil wa Serikali Baraka Mgaya.
Waomba rufaa ambao ni Sabaya, Sylvester Nyegu na Daniel Mbura, waliwakilishwa na Mawakili Mosses Mahuna, Sylvester Kahunduka na Fauzia Mustapha.
“Sisi tuko tayari tunaomba tarehe na wakati muafaka kwa ajili ya kusikiliza,”amesema Kweka
Awali Mawakili wa waomba rufaa wakiongozwa na Mahuna waliwaeleza waandishi wa habari nje ya mahakama kuwa wana sababu zaidi ya 10 ambazo hata hivyo hawakuziainisha.
Oktoba 15 Hakimu Mkazi Mwandamizi, Odira Amworo aliwahukumu Sabaya na wenzake wawili kifungo cha miaka 30 jela kila mmoja baada ya kuthibitika na hatia katika makosa matatu ikiwamo unyang’anyi wa kutumia silaha.