Mamlaka ya Mawasiliano nchini TCRA imeiruhusu Wasafi TV kuanza kurusha matangazo kuanzia Machi 1, 2021, baada ya kupunguza adhabu waliyopewa.

Januari 5, 2021 TCRA ilikifungia kituo hicho kwa miezi sita kutokana na kukiuka kanuni za mawasiliano ya kielektroniki na posta kwa kurusha maudhui yasiyoruhusiwa.

TCRA imeeleza kuwa Januari 21 Wasafi TV iliwasilisha TCRA maombi na vielelezo zaidi ikiiomba mamlaka hiyo kupitia upya uamuzi wake.

Januari 28 wakati wa kusikilizwa kwa maombi yao, kituo hicho kiliwasilisha ushahidi mpya, na kueleza kuwa endapo ungezingatiwa awali, kisingepewa adhabu ya kufungiwa kwa miezi sita.

Kituo hicho kilikiri kurusha matangazo mubashara kinyume na masharti ya leseni yao na kuomba kupunguziwa adhabu waliyopewa.

Taarifa iliyotolewa leo Februari 4, 2021, na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA imeeleza kuwa Wasafi TV itaendelea kutumikia adhabu hiyo mpaka Februari 28, 2021.

Aidha, kituo hicho kimeelekezwa kuzingatia masharti ya leseni ya kutoa huduma za maudhui ya kulipia kwa njia ya televisheni na iwapo kitashindwa, kukataa, au kukaidi uamuzi huo, hatua zaidi za kisheria na kiudhibiti zitachukuliwa dhidi yao.

PICHA: Waziri wa michezo atembelea Azam Complex
Mtihani wa kwanza kwa Didier Gomez Da Rossa