Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza orodha yenye wanafunzi 2,679 ambao wamepata mikopo ya elimu ya juu yenye thamani ya TZS 9.6 bilioni kufuatia kukamilika kwa uchambuzi wa rufaa zilizowasilishwa.

Kati ya wanafunzi hao 1,847 ni wa mwaka wa kwanza ambao mikopo yao ina thamani ya TZS 6.84 bilioni. Wengine 832 ni wale wanaoendelea na masomo lakini hawakuwa na mikopo katika miaka iliyopita. Wanafunzi hao wanaoendelea na masomo wamepata mikopo yenye thamani ya TZS 2.76 bilioni.

Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru amesema orodha ya wanafunzi hao na fedha zao zimetumwa katika vyuo walipo wanafunzi hao.

“Hatua hii inafanya jumla ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza kuwa wamepangiwa mikopo yenye thamani ya zaidi ya TZS 108 bilioni kwa mwaka wa masomo 2017/2018 hadi sasa”, amesema Badru na kufafanua kuwa Serikali imetenga jumla ya TZS 427.54 bilioni kwa ajili ya mikopo hiyo kwa mwaka 2017/2018.

HESLB ilifungua dirisha la rufaa kwa siku saba kuanzia tarehe 13 Novemba, 2017 hadi tarehe 19 Novemba, 2017 ili kuwapa fursa waombaji wote ambao hawakuwa wameridhika na upangaji wa mikopo na kuwasilisha rufaa kupitia vyuo walivyopata udahili.

 

Sanamu la Lionel Messi lavunjwa vunjwa tena
Video: Mwinyi atua kwa Lissu, Wabunge tisa wa Ukawa watajwa kuhamia CCM