Mpango wa wanafunzi kupiga kura za siri ili kuwabaini Walimu wenye mahusiano ya kimapenzi na Wanafunzi maarufu kwa jina la ‘Wakware’ unatarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa mkoani Rukwa.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo amesema, kumekuwa na ongezeko la Walimu wa kiume katika Shule za Msingi na Sekondari kujihusisha katika mapenzi na wanafunzi wao wa kike na kuwasababishia ujauzito.
Ameongeza kuwa, yamekuwepo matukio ya walimu kadhaa wakiwemo Walimu Wakuu wa Shule kukamatwa na kufikishwa Mahakamani wakikabiliwa na mashataka ya kubaka na kuwapatia ujauzito wanafunzi.
Moja ya matukio hayo ni la Mkuu wa Shule ya Msingi Kilambo cha Mkolechi,( Eradi Kapyela) anayetuhumiwa kuwapatia wanafunzi wake 5 ujauzito na amefanikiwa kutoroka na inasemekana amekimbilia kujificha Nchi Jirani ya DRC.
Takwimu za matukio ya Mimba za Utotoni katika Mkoa wa Rukwa kwa kipindi cha 2017 hadi 2019 ni matukio 722 yameripotiwa kati yao 171 walikuwa Shule za Msingi na 551 walikuwa Wanafunzi wa Sekondari.