Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeagiza Clouds TV na Redio kusitisha matangazo yao kwa muda wa siku saba kuanzia kesho Ijumaa ya Agosti 28 hadi Septemba 3, 2020 kwa kosa la kukiuka kanuni za utangazaji na kanuni ndogo za utangazaji za uchaguzi.
Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba amesema, adhabu hiyo inatokana na kukiuka kanuni mbalimbali za utangazaji na kanuni ndogo za wakati wa uchaguzi za mwaka 2015.
Kilaba amesema, Clouds TV na Redio walikiuka kanuni za utangazaji kwa kutangaza wagombea kupita bila kupingwa wakati wenye uwezo wa kutangaza ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
“Iwapo, Clouds Tv itashindwa, au itakataa au itakaidi uamuzi huu basi hatutakuwa na uamuzi mwingine kama TCRA tutachukua hatua zaidi za kisheria na kiudhibiti dhidi yao” amesema Kilaba.
Pia, Clouds Fm imeagizwa kuomba radhi kwa watanzania katika kipindi chote cha adhabu.
Katika hatua nyingine Kilaba ameviasa vyombo vyote vya habari kuzingatia sheria katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.