Serikali ya Russia imekataa kutii amri ya Mahakama ya Umoja wa Mataifa ya kusimamisha uvamizi wake nchini Ukraine baada ya majaji hao wa The Hague kutangaza uamuzi wao.
Msemaji wa serikali hiyo ya Kremlin, Dmitry Peskov alisema, “Hatuwezi kuutekeleza uamuzi huu,” na kuwa pande zote Russia na Ukraine walitakiwa kukubaliana jinsi ya kutekeleza uamuzi huo
“Hakuna kuridhia kunakoweza kuonekana katika shauri hili,” alisema Peskov.
Hivi karibuni Mahakama ya Kimataifa ya Umoja wa Mataifa jana iliamua kuwa Russia isimamishe mara moja shughuli zake za kijeshi ilizozianza Februari 24 ndani ya mipaka ya Ukraine.
Ukraine iliishtaki Russia kwenye mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa baada ya Rais Vladimir Putin kuanza uvamizi huo wa kijeshi.
Peskov alidai kuwa ujumbe wa Russia katika mazungumzo hayo na serikali ya Kyiv kwa ajili ya kumaliza vita ulikuwa unaonyesha utayari kwa kiwango kikubwa kuzidi wenzao katika majadiliano.
Mpaka sasa jumla ya watoto takribani 97 wa Ukraine wamefariki dunia tangu kuanza kwa vita kati ya nchi hiyo na Russia, Rais Volodymyr Zelensky amesema katika hotuba yake kwa bunge la Canada.