Makamu wa Rais wa Kenya, William Ruto amejibu tetesi zilizosambazwa na wanasiasa wenzake kuwa alimpiga kofi Rais Uhuru Kenyatta, huku wengine wakidai hakutekeleza bali alitishia kufanya kitendo hicho.
Akizungumza hivi karibuni, kupitia kituo cha runinga cha Ktn kwenye mahojiano yaliyopewa jina la ‘Ruto Tells It All’ (Ruto anayasema yote), mwanasiasa huyo anayewania nafasi ya urais kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Agosti 31 mwaka huu, alikanusha vikali tetesi hizo.
“Hiyo ni hotuba ya kutengeneza, hivi kweli unadhani unaweza kumpiga kofi Rais? Hakuna mtu anaweza kumpiga kofi Rais kwakweli, ninamaanisha kweli kabisa,” alisema Ruto kwa msisitizo.
Hata hivyo, Mwanasiasa huyo alieleza kuwa katika kipindi alichotumikia kama msaidizi wa Rais Kenyatta, alipitia udhalilishaji wa hali ya juu ambao hakuna mtu angeweza kuuvumilia.
“Naomba nikwambie kweli, udhalilishaji niliofanyiwa na Bosi wangu, hakuna mtu angeweza kuuvumilia.
Akieleza kuhusu mkasa mmoja, Ruto alisema kuwa miaka mitatu iliyopita Rais Kenyatta alimfukuza kwenye Baraza la Usalama la Taifa.
“Rais aliniondoa kwenye orodha ya wanaoshiriki Baraza la Usalama la Taifa kwa sababu nilikuwa nauliza maswali magumu, ikiwa ni pamoja na matukio ya mauaji yanayofanywa na mifumo ya Serikali,” alisema Ruto.
Aidha, Ruto alisema kuwa Rais Kenyatta aliacha kuzungumza naye, na hata Maaskofu walipotaka kuwasuluhisha kiongozi huyo wa nchi alikataa kukaa pamoja naye.
Hata hivyo, Rais Kenyatta amekuwa akieleza kuwa Ruto alikuwa anamkosea heshima mara kadhaa.
Akizungumza na viongozi wa dini katika eneo la Mlima Kenya, Rais Kenyatta alisema kuwa endapo Ruto na timu yake wangempiga kofi katika shavu la kushoto, angewageuzia na shavu la kulia pia.
Katika uchaguzi wa mwaka huu, Rais Kenyatta anamuunga mkono mgombea wa upinzani, Raila Odinga.