Naibu Rais wa Kenya, William Ruto amepuzilia mbali wito wa baadhi ya viongozi wa eneo la Magharibi ambao wanamtaka kuzika ndoto zake za kuwania urais na kumuunga mkono mwanasiasa Musalia Mudavadi.
Ruto ameeleza hayo wakati akiwahutubia waombolezaji siku ya Jumamosi, katika Shule ya Msingi ya Nakhwana, Bungoma wakati wa mazishi ya Maurice Mabonga ( baba yake Mbunge wa Bumula Mwambu Mabonga), ambapo amesema hawezi kumuunga mkono Mudavadi wala Moses Wetang’ula kwani wote wanatoka katika familia za matajiri.
“Kiongozi wa ANC, Musalia Mudavadi ni mtoto wa waziri hata Wetang’ula hapa naambiwa ni mtoto wa mzee wa kijiji cha Likuru na huku baba yangu alikuwa maskini bila hata kuwa mzee wa kjiji na mwataka nimuunge mkono. Hiyo ni ungwana kweli?” amesema Ruto.
Ruto ambaye ni Mwanachama wa Jubilee pia alihamasisha vuguvugu lake la ‘hustler’ na kusisitiza kwamba watoto wanatakiwa kutiwa motisha ya kuwa viongozi nchini licha ya kulelewa katika umaskini.
Aidha, Ruto amekosoa ukaribu wa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa Upinzani, Raila Odinga akidai kuwa ukaribu huo umekuwa chanzo cha utawala mbaya wa serikali ya Jubilee.
“Wakati wa muhula wetu wa kwanza ofisini, tulifanya miradi nyingi. Tulijenga barabara, tukawekea watu umeme na maji, tukajenga taasisi za ufundi hadi huu muhula wa pili ambao umetekwa nyara na siasa za handisheki na BBI,” amesema Ruto.