Rais wa Kenya, William Ruto amesema kauli mbiu iliyozoeleka duniani ya kujenga upya kwa ubora baada ya janga la COVID-19 linapaswa kuongezewa sentensi ili ikamilike vizuri na kuwa na maana ya kufikia wale walio chini zaidi.
Akihutubia kwa mara ya kwanza mjadala Mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA77 jijini New York, Marekani, Ruto amesema kauli hiyo lazima ikamilike kwa kusema Kujenga Upya kwa Ubora kuanzia chini.
Amesema, Kauli ya kujenga upya kwa ubora inalenga kujifunza kutoka makosa ya awali na kujenga uhimili na mnepo na kwamba anadhani ipo fursa bora ya kuzingatia kauli hii kwa kuipaisha zaidi kwa neno na vitendo kwa kuongeza B nyingine (Building Back Better from the Bottom), akimaanisha Tujenge Upya kwa ubora kuanzia chini.
Rais Ruto amesema, kujenga upya kuanzia chini ni jambo jema kwa kuwa linahusisha kundi kubwa la wanaochangia kwenye uchumi ambalo limeenguliwa huku akiongeza kuwa, “Watu bilioni waliooenguliwa wanahaha kujipatia kipato cha siku ili waweze kuishi kwenye maeneo ambayo hayana fursa.”
“Vipaji vyao, matumaini, mnepo na nguvu walizo nazo mara nyingine hutambulika kama kupambana, wapambanaji hawaonwi na watunga será lakini hawakati tamaa na hawafikiwi na huduma nyingi za umma, wapambanaji hawapuuzii chochote, wanapitia magumu na hatimaye mara nyingi hufanikiwa, ” amefafanua Ruto.
Hata hivyo, Rais Ruto ametumia pia hotuba yake kuelezea jinsi alivyojiandaa kunufaika na uchumi wa buluu, au ule unaotokana na matumizi ya rasilimali za bahari, akisema wamejifunza mengi baada ya mkutano wa mwaka 2018 wa Umoja wa Mataifa uliofanyika nchini Kenya kuhusu faida za ukanda bahari.