Rais wa Kenya, William Ruto anatarajiwa kutoa hotuba yake ya kuapishwa kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA), hii leo septemba 21, 2022 Jijini New York, nchini Marekani.
Hayo, yamesemwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Kenya, Hussein Mohamed ambapo ameeleza kuwa Ruto anatarajiwa kupanda jukwaani saa 9.00 Alasiri EAT kutoa taarifa ya kitaifa ya Kenya.
Katika hotuba yake ya kwanza kwa Umoja wa Mataifa, Ruto atalenga kukuza Sera ya Kigeni ya Kenya katika mfumo wa kimataifa, kuimarisha ushiriki wa kutimiza malengo ya maendeleo endelevu na uongozi wa kimataifa katika masuala yanayoibuka kama vile mabadiliko ya hali ya hewa.
Ruto pia, anatarajiwa kuongoza azma ya Kenya ya kuunganisha uhusiano na Marekani wa nguzo 5 za ushirikiano wa kimkakati kupitia mazungumzo baina ya nchi mbili na anahudhuria mkutano huo akitokea kuhudhuria mazishi ya Malkia Elizabeth Septemba 19, huko Westminster, Uingereza.
Katika mkutano huo, Ruto ameandamana na mkewe Rachel Ruto na washirika wake wa karibu Seneta Kipchumba Murkomen, Mbunge Ndindi Nyoro, Katibu Mkuu Tawala Wizara ya Masuala ya Kigeni Ababu Namwamba, miongoni mwa wengine.
Akiwa nchini Marekani, Ruto pia anatarajiwa kufanya mazungumzo na wawakilishi wakuu wa wafanyabiashara wa Marekani ili kutetea ongezeko la biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.