Makamu wa Rais wa Kenya William Ruto amethibitisha rasmi kuwa chama kipya cha UDA kitaingia katika ushirikiano na chama cha Musalia Mudavadi cha Amani National Congress (ANC) na chama cha FORD-Kenya kinachoongozwa na Moses Wetangula.
Akiwahutubia wajumbe wa chama cha ANC katika ukumbi wa Bomas of Kenya, Ruto alifichua kwamba alifanya majadiliano ya muda mrefu yenye mafanikio, yaliyolenga kuunda muundo wa kisiasa, na wawili hao.
Alithibitisha kuwa muungano wao mpya utafanya mikutano mingi kote nchini kuanzia wiki ijayo na kuwa wataanza safari yao mpya ya kisiasa Jumatano mjini Nakuru kabla ya kuelekea Magharibi mwa Kenya siku ya Ijumaa na Kenya ya Kati wikendi.
“Tumekuwa na mazungumzo na ndugu zangu na kukubaliana kwamba Kenya ni kubwa kuliko sisi sote, tunakwenda kujitoa mhanga. Tumeanzia Bomas na kituo chetu kingine kitakuwa Nakuru.” Ruto alisema.
Kuingia kwa Ruto katika muungano huo hata hivyo ni kubatilisha msimamo wake mkali wa awali kuhusu ushirikiano wa kisiasa kabla ya uchaguzi ambapo amesisitiza mara nyingi kwamba hakuwa tayari kushirikiana na vyama ambavyo alivitaja kuwa vidogo na vya kikabila.
Kiongozi huyo nambari mbili nchini Kenya, kwa muda mrefu amekuwa akiwashinda viongozi wanaotaka kuungana naye kuvunja vyama vyao na kujiunga na vazi lake la UDA.
Hata hivyo Vinara wa Muungano wa One Kenya Alliance (OKA) Gideon Moi wa chama cha KANU na mwenzake wa Wiper Kalonzo Musyoka waliondoka katika hafla hiyo baada ya William Ruto kuwasili katika ukumbi huo kuhudhuria hafla hiyo ambayo Mudavadi alisema kuwa itatetemesha siasa za taifa hili.
Wawili hao hawakuelezea sababu ya kuondoka kwao lakini inashukiwa kuwa kisa cha kuhisi kusalitiwa kwa sababu wao pia wanawinda kiti cha urais katika uchaguzi mkuu Agosti 9, 2022.
Kinara mwingine wa OKA Moses Wetangula wa chama cha Ford Kenya hata hivyo alisalia katika ukumbi huo akikaa mkabala na Ruto.
Ruto aliwasili katika ukumbi huo mchana wa Jumapili, Januari 23, muda mfupi tu baada ya kufahamika kuwa alikuwa amealikuwa amealikuwa katika mkutano huo.