Mbunge wa Gatundu Kusini Nchini Kenya, Moses Kuria ametabiri kuwa naibu rais William Ruto na kinara wa ODM Raila Odinga watafanya serikali ya Umoja ‘handisheki’ baada ya uchaguzi wa Agosti.

Moses Kuria amesema hayo wakati wa sherehe yake kukaribishwa nyumbani februari 19, iliyofanyika uwanja wa Thika, akiwataka wakazi wa Mt Kenya kutoshawishika na siasa za wawili hao.

Alisema wakazi wanafaa kujua mgao wao utakuwa ni upi ndani ya serikali ya Ruto au ya Raila na wala si kuwapa kura zao bila matakwa.

“Eti sisi tunaombwa kura ya Kiambu, Murang’a na Nyeri bure. Si tuwaambie kwanza wawekelee, hawa watapata kura na ushindi lakini sisi tutabaki na nini? Watafanya handisheki baada ya uchaguzi. Watasalimiana, si ata hapo awali walikuwa pamoja? Wakiungana tena sisi tutabaki wapi? Kwa sababu ninajua wataungana, lazima watarudiana tu. Sia afadhali tujipange mapema, wawekelee yetu mapema,” alisema Kuria.

Aidha mbunge huyo Kuria alipuuza ripoti ambazo zimekuwepo kuwa Rais anapanga kuendelea kushikilia mamlaka licha ya kuhudumu kwa mihula miwili na amesema Rais Uhuru Kenyatta ataondoka katika siasa baada ya uchaguzi wa mwezi Agosti, kwa kuwa yuko tayari kwenda nyumbani.

Mbunge huyo alisema alizungumza na Rais kuhusu mpango wake baada ya muhula wake kukamilika. “Mimi mnajua ndiye mbunge wa Uhuru Kenyatta, mnajua mimi huwa siogopi kumwambia ukweli. Mimi nimemuuliza Rais Uhuru Muigai Kenyatta iwapo akimaliza muhula wake miezi wa nane ataenda nyumbani Akaniambia hataongeza hata dakika moja. Na kwa sababu mimi ndiye mbunge wake, mimi ndio nitakuwa kwa kamati ya kumwalika pale Gatundu,” alisema Kuria.

Alisema Rais Uhuru yuko tyaari kuacha mamlaka kwa yule ambaye ataibuka mshindi wa uchaguzi wa mwezi Agosti. “Atatoka Ikulu na kuenda mpaka Kasarani ambapo atapewa mamlaka. Yule ambaye mtamchagua ndiye Uhuru atamkabidhi mamlaka, Na sasa kwa sababu amekubali kuenda nyumbani, tumpeleke nyumbani kwa njia ya heshima. Yeye si malaika, lakini kwa sababu amekubali kuenda nyumbani tufanye hivyo kwa heshima,” alisema.

Uchaguzi Mkuu wa Kenya unatarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka 2022, ambapo mpaka sasa vinara wa uchaguzi huo ni Naibu Rais William Ruto na Kiongozi mkuu wa cahma cha ODM, Raila Odinga ambapo Duru za kisiasa zinasema kuwa, Odinga ndie anapigiwa debe na Rais wa sasa wa Kenya Uhuru Kenyatta.

Makamu wa Rais Dkt Mpango aifariji familia ya Malecela
Mapya yaibuka kuhusu njama za kumuua Rais Uhuru Kenyatta