Kocha Msaidizi wa Ruvu Shooting Mohamed Nakuchema amekiri mambo kuwa magumu kwa upande wa klabu hiyo, kutokana na changamoto za ushindani wanazokutana nazo kwenye Michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, msimu huu 2022/23.
Nakuchema ametoa kauli hiyo alipozungumza na Waandishi wa Habari leo Ijumaa (Novemba 18) majira ya Mchana, kuelekea mchezo dhidi ya Simba SC utakaopigwa kesho Jumamosi (Novemba 19), Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Kocha huyo amesema changamoto za ushindani katika Ligi zimepelekea kikosi chao kupoteza michezo mingi hadi sasa, hali ambayo imeendelea kuwapa wakati mgumu wa kupambana na kubuni mbinu zitakazowaondoa kwenye nafasi za chini.
“Ligi imekuwa ni ngumu sana nyie ni mashahidi wakubwa wa hilo, tunakosa matokeo kwenye michezo mingi lakini tuwaahidi kufanya vizuri zaidi.”
“Tunafanyia kazi hasa eneo la finishing ili tujitengenezee kupata matokeo mazuri, wachezaji watakaokosekana ni wale wale walioenda kozi za kikazi.” amesema Nakuchema
Ruvu Shooting watakaokuwa wenyeji wa Simba SC kesho Jumamosi (Novemba 19), wapo katika nafasi ya 13 wakiwa na alama 11 walizozipata kwenye Michezo 12 waliocheza hadi sasa, wakishinda mitatu, wakidroo miwili na wameshapoteza saba.
Kwa upande wa Simba SC ipo nafasi ya tatu kwenye Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 24, ikitanguliwa na Azam FC yenye alama 26 sawa na Young Africans inayopepea kileleni.