Kitendo cha kuifungia Young Africans dhidi ya Ruvu Shooting kimemuibua Nahodha na Beki wa klabu hiyo Bakari Nondo Mwamnyeto ambaye kwa kipindi kirefu alikosa nafasi ya kucheza katika kkosi cha kwanza.
Mwamnyeto alifunga bao lake la pili msimu huu, akitangulia kufanya hivyo kwenye mchezo wa Mzunguuko wa Pili wa Ligi Kuu dhidi ya Polisi Tanzania jijini Arusha.
Akizungumzia hatua ya kufunga bao katika mchezo wa juzi Jumatano (Oktoba 03) dhidi ya Ruvu Shooting, Beki huyo amesema amefarijika kuwa miongoni mwa wafungaji walioipa Young Africans ushindi kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliyopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Bao lingine la Yanga katika mchezo huo, lilifungwa na Feisal Salum ‘Fei Toto’, hivyo kuifanya timu hiyo iendelee kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 13 sawa na Simba SC iliyopo kileleni kutokana na tofauti kubwa ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Mwamnyeto amesema msimu huu ukipata nafasi ya kufunga unapata matumaini kikosini kutokana na ushindani wa namba uliopo.
“Nimepata faraja kufunga goli langu la pili msimu huu, tunafahamu ugumu wa ligi yetu, hivyo ukipata nafasi kama hiyo inazidi kukupa hamasa ya kuipambania timu,” amesema Mwamnyeto.
Amesema baada ya kuiwezesha timu yake kupata alama tatu dhidi ya Ruvu Shooting, sasa anaelekeza nguvu kwenye mchezo wao wa kimataifa dhidi ya Al Hilal ya Sudan, utakaopigwa Oktoba 8, mwaka huu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
“Kwa sasa akili yangu ninaielekeza kwenye mchezo wetu wa Ligi ya Mabingwa Afrika, lengo ni kuipa mafanikio timu yangu kwenye uwanja wa nyumbani,” amesema nahodha huyo ambaye katika nafasi ya beki wa kati amekuwa akipata wakati mgumu wa kuanza kikosi cha kwanza dhidi ya Dickson Job na Yannick Bangala.”
Amesema atashirikiana na wachezaji wenzake kufuata maelekezo wanayopewa na Benchi lao la Ufundi ili wapate matokeo mazuri Jumamosi dhidi ya Al Hilal.
Mwamnyeto amesema mchezo huo unatarajiwa kuwa mgumu na wenye ushindani na kudai wataingia uwanjani kwa tahadhari kubwa.
Endapo Young Africans itapata matokeo ya jumla katika mchezo huo na ule wa ugenini Oktoba 16, mwaka huu, itafuzu hatua ya makundi na timu itakayotolewa itaangukia mechi za mchujo za Kombe la Shirikisho ili kuwania kufuzu hatua ya makundi ya kinyang’anyiro hicho cha pili kwa ubora na utajiri kwa ngazi ya klabu barani Afrika.