Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Jenista Mhagama, ametoa siku moja kwa Mtendaji wa Kijiji cha Bukulu katika Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa kuhakikisha mlengwa wa TASAF kijijini humo, Laurent Chebu anapewa ruzuku yake na kumpatia taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo. 

Jenista ametoa maelekezo hayo wakati akizungumza na walengwa wa TASAF na wananchi wa Kijiji cha Bukulu wilayani Kondoa akiwa kwenye ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wilayani humo.

“Mtendaji nimekuuliza hapa na umekiri kwamba Laurent Kibu hajapata ruzuku yake kwasababu yeye na mwenzeke walikuwa safarini, hivyo ninakupa muda wa kushughulikia suala hili mpaka kesho jioni na unipigie simu wewe mwenyewe kunieleza kuwa mlengwa huyu ameshapewa na wengine ambao bado wapewe ruzuku zao,” amesema Waziri Jenista.

Aidha, amewataka watendaji na waratibu wa TASAF kote nchini kuhakikisha fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya walengwa wa TASAF zinawafikia walengwa kwa wakati, kama ambavyo Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ilivyokusudia.

“Watendaji na waratibu wa TASAF nisingependa kusikia mlengwa wa TASAF hajapewa ruzuku yake, iwe kwasababu ya kutokuwepo wakati wa dirisha au sababu nyingine yoyote ile kwani lengo la TASAF ni kuwawezesha walengwa kuboresha maisha yao,” amesema.

Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika mwaka wa fedha 2021/2022 imetoa kiasi cha shilingi bilioni 2.6 katika Wilaya ya Kondoa kwa ajili ya kutekeleza Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini wilayani humo.

Tukio la uvamizi wa mwanamke Kenya:mmoja ashikwa akitoa pesa kwenye simu ya muathiriwa
Mauaji ya kutisha Burkina Faso