Serikali ya Rwanda imeviagiza Vyama vya Michezo nchini humo kusimamisha mipango yote ya kushiriki katika michezo ya kimataifa itakayochezwa nje ya Rwanda.
Uamuzi huo ni njia ya kupambana na janga la virus vya Corona ambalo limekuwa likienea kote Ulimwenguni kwa kasi.
Moja ya hitimisho lililofikiwa katika mkutano uliofanyika jana Jumanne ni kuzitaka asasi zote kuacha shughuli zote za michezo zilizopangwa kufanywa nje ya Rwanda, haswa katika nchi ambazo zimeathiriwa na ugonjwa huo.
Wizara ya Michezo imeyataka mashirikisho ya michezo kuwasiliana mara moja na CAF na FIFA ili kuzuia kuwekewa vikwazo.
Hii inamaanisha kuwa Rwanda haitasafiri kwenda Cape Verde kwa ajili ya kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON 2021 na pia Mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani CHAN2020 itakayofanyika Cameroon mwezi ujao.