Wanajeshi watano wa Rwanda wamekamatwa baada ya wakazi wa kitongoji cha mji mkuu wa Kigali kudai waliwabaka wanawake walipokua wakitekeleza sheria ya kukaa nyumbani iliyowekwa kote nchini humo ili kuzuia mambukizi ya Covid-19 kusambaa.
Kwa mujibu wa mwandishi wa BBC, Wakazi wa kitongoji cha Nyarutarama wameiambia ofisi ya mwendesha mashtaka wa jeshi kwamba askari waliwapiga wakazi na kuwaibia mali zao.
Ambapo mmoja wa waathiriwa amewambia waandishi wa habari kuwa mnamo tarehe 26 Machi, mwanajeshi aliyekua amejihami kwa silaha aliingia kwa nguvu katika nyumba yake na kumpiga mume wake, alipokua akijaribu kuingilia kati kumzuia askari asimbake.
Serikali ya Rwanda iliweka sheria ya kutotoka nje kote nchini humo ili kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona, lakini baadhi ya wakazi wamekua wakilalamika juu ya ukatili wanaofanyiwa na maafisa wa usalama wanaosimamia utekelezwaji wa sheria hiyo.
Mpaka hivi sasa Rwanda imethibitisha kuwa na visa 84 vya watu wenye maambukizi ya virusi Corona.