Shirika la Upelelezi la Rwanda (RIB), limefanikisha kuwakamata watuhumiwa 57 wa ugaidi wakiwa wamejificha kwenye msitu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Msemaji wa RIB, Dominique Bahorera amewaambia waandishi wa habari kuwa watuhumiwa hao wamekamatwa Ijumaa, Julai 17, 2020 wakiwa msituni. Alisema kuwa walikamatwa na majeshi ya DRC ambayo yaliwakabidhi Rwanda.
Ameeleza kuwa kati ya watuhumiwa hao kuna majenerali watano wa makundi mbalimbali ya kigaidi na kwamba wote watafikishwa kwenye mahakama ya kijeshi isipokuwa raia watakaopelekwa kwenye mahakama za kiraia.
Watuhumiwa hao ni kati ya wanafamilia wa makundi ya kigaidi ya Rwanda ikiwa ni pamoja na National Liberation Front (FLN), RUD Urunana, the Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR), Rwandan Movement for Democratic Change (MRCD) na P5, kwa mujibu wa Bahorera.
Ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa imelihusisha kundi la P5 na Kayumba Nyamwasa aliyekuwa Kigogo katika Jeshi la Rwanda.
Kwa upande wa kundi la FLN, Machi 2019 lilidai kuwa limefanikiwa kukamata mikoa ya Rwanda karibu na msitu wa Nyungwe, eneo ambalo linapakana na Nyamagabe na Wilaya ya Nyaruguru, Kusini mwa Rwanda.
Kauli ya Polepole kitendawili kwa viongozi waliochukua fomu, ‘umetukimbia mtoni’