Meneja mpya wa klabu ya Arsenal Unai Emery huenda akawauza wachezaji saba katika kipindi hiki cha dirisha la usajili wa majira ya kiangazi, ili kufanikisha mpango wa kufanya usajili wa wachezaji wengine wawili, ambao watajiunga na The Gunners kabla ya kufungwa kwa dirisha.

Meneja huyo kutoka nchini Hispania tayari ameshawasajili wachezaji watano tangu alipowasili klabuni hapo, ambao ni Lucas Torreira, Sokratis Papastathopoulos, Bernd Leno, Stephan Lichtsteiner na Matteo Guendouzi.

Kwa mujibu wa tovuti ya Goal, Unai amedhamiri kufanya mpango huo, kwa minajili ya kukiboresha zaidi kikosi chake ambacho msimu ujao, kinatarajiwa kuwa na ushindani tofauti na kilivyokua chini ya meneja Arsene Wenger.

Dhumini kubwa kwa meneja huyo ni kutaka kufanya usajili wa mchezaji anaecheza nafasi ya ushambuliaji wa pembeni pamoja na beki wa kushoto.

Miongoni mwa wachezaji ambao wanatajwa huenda wakauzwa kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili ni Shkodran Mustafi, Nacho Monreal, Petr Cech, David Ospina, Danny Welbeck, Lucas Perez na Carl Jenkinson.

Katika hatua nyingine kiungo wa Arsenal Kelechi Nwakali ameuzwa kwa mkopo kwenye klabu ya FC Porto ya Ureno.

Kiungo huyo mzaliwa wa nchini Nigeria mwenye umri wa miaka 20, alijiunga na Arsenal mwaka 2016, na msimu uliopita alipelekwa kwa mkopo kwenye klabu ya MVV Maastricht ya nchini Uholanzi.

Nwakali ataitumikia FC Porto kwa mkopo hadi mwishoni mwa msimu wa 2018/19.

Wakati huo huo Unai Emeri amesema mpaka sasa hawajapokea ofa kutoka kwa wababe wa Stamford Bridge (Chelsea), inayomlenga mlinda mlango Petr Cech, ambaye yupo kwenye orodha ya wachezaji ambao huenda wakauzwa.

Cech anakabiliwa na changamoto ya kuwania nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Arsenal, baada ya kusajiliwa kwa mlinda mlango kutoka nchini Ujerumani Bernd Leno, aliyetokea Bayer Leverkusen  kwa ada ya pauni milioni 19.

SUA yagundua mwarobaini tatizo la nguvu za kiume
Ridhiwani azungumzia kifo cha babu yake

Comments

comments