Askari wanne pamoja na raia watatu wameuawa baada ya vikosi vya maji vya jeshi la Uganda na askari wa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kushambuliana, kwenye eneo la Ziwa Edward lililo kwenye mpaka wa nchi hizo mbili.
Mtawala wa eneo la Mkoa wa Beni, Donat Kibwana ameeleza kuwa tukio hilo lilitokea Alhamisi wiki hii akieleza kuwa vikosi vya Uganda vinavyofanya doria vilianzisha mashambulizi.
“Boti ya Uganda ilizama na wanajeshi wanne pamoja na raia watatu walikufa. Kwa upande wa Kongo, mwanajeshi mmoja na raia mmoja walijeruhiwa,” Kibwana anakaririwa.
Alisema kuwa mashambulizi kati ya vikosi vya nchi hizo mbili yameongezeka zaidi mwezi huu.
Jumatano wiki hii, vikosi vya doria vya Uganda viliwakamata wavuvi 18 wa Kongo waliokuwa wanafanya shughuli za uvuvi katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, vikosi vya Kongo vinatekeleza jukumu la kulinda eneo hilo dhidi ya waasi kutoka nchini Uganda na Rwanda.
Eneo hilo la Mashariki mwa Kongo limekuwa likishuhudia migogoro na mashambulizi tangu mwaka 1990.