Serikali nchini, imesema mfumuko wa bei nchini Tanzania ni wa kiwango cha chini zaidi ikilinganishwa na nchi jirani za Kenya, Rwanda na Uganda na kwamba bei za vyakula katika nchi nyingi zimepanda.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt, Ashatu Kijaji na kuongeza kuwa, bei ya Maharage imepanda kutoka Shilingi 215,193 kwa gunia la kilo 100 mwezi Februari, 2022 hadi kufikia Shilingi 301,297 kwa mwezi Februari, 2023 sawa na ongezeko la asilimia 40.
Dkt, Ashatu ambaye alikuwa akiwasilisha bajeti ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, amesema wastani wa bei ya mahindi kwa gunia la kilo 100 imeongezeka kutoka Sh 90,330 mwezi Februari, 2022 hadi kufikia Sh 115,141 mwezi Februari, 2023 sawa na ongezeko la asilimia 27.5.
“Wastani wa bei ya mchele kwa gunia la kilo 100 imeongezeka kutoka Sh 216,738 mwezi Februari, 2022 hadi Sh 291,819 mwezi Februari, 2023 sawa na ongezeko la asilimia 34.6 na kutokana na mabadiliko ya tabianchi na athari mazao muhimu ya chakula kama vile mchele, mahindi, maharage na viazi mviringo yanahitajika kwa wingi nje ya nchi.
Tanzania kiwango cha mfumuko wa bei ni asilimia 4.9 kwa mwezi Januari 2023 ikilinganishwa na asilimia 9.1 nchini Kenya, asilimia 10.4 Uganda na asilimia 21.7 nchini Rwanda kwa mwezi Januari, 2023. Aidha, katika mwaka 2022 mfumuko wa bei ulikuwa kwa wastani wa asilimia 4.3.