Benchi la Ufundi la Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Simba SC, limefunguka kuhusu kadi nyekundu ambazo zimetolewa kwa wapinzani wao tangu kuanza kwa msimu huu 2021/22.
Katika michezo mitano ya Simba SC waliyocheza hadi sasa, wapinzani wao wanne walimaliza wakiwa pungufu kufuatia utovu wa nidhamu waliouonyesha ndani ya dakika 90.
Akizungumzia hali hiyo aliyekua Kaimu Kocha Mkuu wa Simba SC Hitimana Thierry, amesema wapinzani wao wamekua wakipata kadi nyekundi kutokana na kuonyesha mchezo wa kukama na kucheza kwa nguvu nyingi wakati wote.
Hitamana amesema kuwa moja ya jambo gumu ambalo wamekuwa wakikutana nalo tangu kuanza kwa msimu huu ni wachezaji wao kucheza kwa kukamiwa na wapinzani wakiwa na lengo la kuwaumiza jambo ambalo limekuwa likiwarudisha nyuma katika kupata matokeo.
“Unajua kumekuwa na mambo mengi sana ambayo yanaendelea katika mechi zetu lakini kubwa tumekuwa tukikamiwa katika kila mchezo kwa wapinzani kucheza soka la nguvu ambalo limepelekea kuwa na kadi nyingi nyekundu kwenye mechi zetu.
“Kiukweli inaumiza kwa sababu inaonyesha hii ni dhamira ya makusudi ambayo inatukwamisha wakati mwingine kwa sababu siyo kitu rahisi kuwakosa wachezaji muhimu kwenye mechi zetu, nadhani ni wakati wa timu kucheza mpira siyo kukamiana,” amesema Hitimana.
Wapinzani wa Simba SC waliopata kadi hadi kumalizika kwa mzunguuko watano wa Ligi Kuu Tanzania Bara ni Dodoma Jiji FC, Polisi Tanzania FC, kisha katika mchezo wa Coastal Unioni na mwisho ukiwa wa Namungo FC.