Maafande wa JKT Tanzania wamekamilisha usajili wa winga Sixtus Sabilo wakimpa mkataba wa miaka miwili na sasa ataungana na aliyekuwa staa mwenzake ndani ya kikosi cha Mbeya City, Hassan Nassoro ‘Machezo’ kuwatumikia maafande hao.

Wawili hao wote wametua JKT katika dilisha kubwa hili la usajili lakini kabla ya hapo waliwindwa na timu nyingine tofauti ambapo Machezo alitakiwa na Simba SC na Singida Fountain Gate huku Sabilo alihitajika na Ihefu FC sambamba na Tanzania Prisons.

Kutua kwao JKT ni pigo kwa Mbeya City iliyoshuka daraja kwani wawili hao msimu uliopita walikuwa ni muhimili mkubwa wa timu hiyo ambapo Sabilo alifunga jumla ya mabao tisa na kutoa pasi za mabao nane, huku Machezo akifunga mabao mawili na asisti mbili kwenye ligi.

Machezo ameeleza kufurahi kuungana tena na Sabilo na kuahidi kuendeleza ushirikiano wake.

Sabilo ni mchezaji mzuri na mpambanaji, ni furaha kuwa naye kikosini naamini kwa pamoja tutafanya vizuri,” alisema Machezo.

Aidha kocha mkuu wa JKT, Malale Hamsini alisema usajili waliofanya msimu huu umezingatia matakwa ya Ligi Kuu.

“Kuna baadhi ya wachezaji tulikuwa nao tukiwa Championship tumewaacha na tumesajili wapya. Tunachokifanya ni kutaka kuendana na kasi ya Ligi Kuu na tunaamini kila mchezaji tuliyemsajili atajituma na kuhakikisha tunafikia malengo yetu,” amesema Malale.

Mastaa wengine waliosajiliwa JKT ni pamoja na Saidi Ndemla, George Wawa, Aman Kyata, Deusdedith Okoyo, Ismail Kader, Danny Lyanga, David Bryson najuzi Jumatatu (Julai 31) walikuwa katika Hospitali ya Mkoa ya Shinyanga wakipatiwa vipimo vya Afya kabla ya kuanza mikiki ya ligi.

Bedie aaga Dunia akiwa na umri wa miaka 89
Dkt. Tax kufungua Ubalozi wa Tanzania nchini Algeria