Rais John Magufuli na mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) anayemaliza muda wake, amezitaka nchi wanachama kupitia sekretarieti kuangalia uwezekano wa kuimarisha mfuko wa fedha za dharura katika kupambana na majanga kama ilivyo sasa ambapo Dunia inakabiliwa na CORONA
Sambamba na hayo Rais Magufuli amezitaka Jumuiya za Kimataifa kuzisamehe au kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa nchi za Afrika hususa nyakati za majanga.
Aidha amezitaarifu nchi hizo kuwa katika kipindi cha uongozi wake, SADC imefanikiwa kuongeza upatikanaji wa umeme kwa zaidi ya megawatts 3500 lengo likiwa ni kuendelea kuimarisha mkakati wa kikanda wa uanzishwaji viwanda sambamba na kushuhudiwa mikataba mbalimbali ikisainiwa.
Pia ameweka bayana kuhusu mafanikio ya kuridhiwa kwa matumizi ya lugha ya Kiswahili katika mikutano ya SADC na kufundishwa kwa baadhi ya nchi sambamba na kulipigia kelele suala la Zimbabwe kuondolewa kwa vikwazo ambalo limeanza kutoa nuru kwa Umoja wa Ulaya kuonesha njia.