Mshambuliaji kutoka nchini Senegal Sadio Mane amesaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia klabu ya Liverpool, ambao utamuwezesha kufanya kazi chini ya majogoo hao wa jiji, hadi mwaka 2023.
Mane mwenye umri wa miaka 26, amekubali kufikia maazimio hayo ya kusaini mkataba mpya, baada ya kukamilisha mazungumzo na viongozi wa Liverpool, ambao bado wameonyesha kuwa tayari kufanya kazi na mshambuliaji huyo.
Mkataba wa awali wa mshambuliaji huyo aliyesajiliwa na Liverpool mwaka 2016 akitokea Southampton ya England kwa ada ya Pauni milioni 34, ulikua unafikia kikomo mwaka 2021.
“Nimefurahishwa na hatua ya kusaini mkataba mpya, nitaendelea kuwa hapa kwa kipindi kingine cha miaka mitano,” alisema Mane alipohojiwa na mwandidhi wa tovuti wa Liverpool FC.
“Ni hatua kubwa kwangu kuendelea kuwa hapa, ninaamini kuna jambo kubwa viongozi wangu wmaeliona kwangu, wanahitaji tuendelee kusaidiana katika kusaka mafanikio ya klabu hii, na mimi bila ajizi nimefanikisha hatua ya kusaini mkataba mpya.”
“Nafahamu kiu kubwa ya klabu ya Liverpool ni kutwaa mataji, na imedhihirika kiu hiyo inapaswa kumalizwa na hatua ya uwepo wangu na usaidizi wa wachezaji wengine, ambao kila siku tumekua tukifanya kazi kwa ushirikiano mkubwa.”
Mshambuliaji Sadio Mane na wenzake Mo Salah na Firminho.
Hatua ya kusaini mkataba mpya, inamfanya Mane aungane na washambuliaji wenzake klabuni hapo Mohamed Salah na Roberto Firmino ambao siku za nyuma walikamilisha taratibu za kusaini mikataba mipya.
Mkataba mpya wa Mane, utamuwezesha kulipwa mshahara wa Pauni 150,000 kwa juma.
Katika msimu wake wa kwanza, Mane alifaniiwa kuifungia Liverpool mabao 20, hali ambayo ilichochea kutangwazwa kuwa mchezaji bora wa klabu wa klabu hiyo ya Anfield.