Mshambuliaji Sadio Mane huenda akaanza kwenye kikosi cha Liverpopol kitakachowakabili mabingwa wa soka nchini Ufaransa PSG usiku wa leo kwenye mchezo wa ligi ya mabingwa barani Ulaya, baada ya meneja wa klabu hiyo ya Anfield Jurgen Klopp kupokea taarifa njema kutoka kwa madaktari.
Mshambuliaji huyo alimaliza mchezo wa ligi ya England mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Watford akiwa na maumivu ya mwilini, hali ambayo ilizusha hofu huenda akaukosa mchezo wa leo.
Klopp amewaambia waandidhi wa habari jijini Paris kuwa, Mane alifanya mazoezi na wachezaji wenzake kabla ya safari ya jijini humo, na amesafiri na kikosi cha The Reds tayari kwa mchezo huo ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka duniani kote.
Hata hivyo meneja huyo kutoka nchini Ujerumani hajatoa uhakika kama ataweza kumuanzisha mshambuliaji huyo, ambaye ameshafunga mabao saba msimu huu, zaidi ya kuthibitisha yupo Fit.
Wakati Liverpool wakifurahia taarifa hizo, upande wa wapinzani wao PSG nao wanachagizwa na taarifa za uwezekano wa kuwatumia washambuliaji wao hatari Neymar na Kylian Mbappe, ambao walipatwa na majeraha wakiwa na vikosi vya timu zao za taifa juma lililopita.
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinadai kuwa, wawili hao wamefanyiwa vipimo na imethibitika wapo tayari kucheza mchezo dhidi ya Liverpool, ambao utaamua hatma yao ya kusonga mbele, ama kuendelea kusubiri.
Neymar aliumia mguu wa kulia alipokua kwenye mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Cameroon, ili hali Mbappe alipatwa na maumivu wa bega la mkono wa kulia akiwa kwenye mtanange dhidi ya Uruguay.
Hata hivyo washambuliaji hao hawakuwepo kwenye kikosi cha PSG kilichocheza mchezo wa ligi ya Ufaransa mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Toulouse, waliokubali kufungwa bao moja kwa sifuri.
Liverpool na PSG zote zinahitaji ushindi katika mchezo wa hii leo ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu hatua ya 16 bora.
Mpaka sasa masimamo wa kundi C unaonyesha SSC Napoli na Liverpool zinaongoza kwa kuwa na alama sita, zikifuatiwa na PSG wenye alama tano na Star Belgrade wanaburuza mkia kwa kuwa na alama nne.