Majogoo wa jiji Liverpool wana matarajio makubwa ya kumkaribisha mshambuliaji wao kutoka nchini Senegal Sadio Mane, katika mchezo wa leo wa ligi ya mabingwa barani Ulaya hatua ya makundi dhidi ya Red Star Belgrade.
Mane mwenye umri wa miaka 26, hakuwa sehemu ya kikosi cha Magojoo hao wa Anfield katika mchezo wa ligi mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Huddersfield, kufuatia jeraha la mkono ambalo alilipata akiwa katika majukumu ya kuitumikia timu yake ya taifa.
Meneja wa Liverpool Jurgen Klopp amethibitisha uwezekano wa kumtumia Mane katika mchezo wa leo, lakini akakiri kuwakosa viungo Jordan Henderson pamoja na Naby Keita.
Amesema Henderson anasumbuliwa na majeraha ya misuli ya paja, hali ambayo itaendelea kumuweka nje ya kikosi chake hadi kwenye mchezo wa ligi kuu wa mwishoni mwa juma dhidi ya Cardiff City ambao watasafiriki kuelekea mjini Liverpool.
“Majeraha ya Henderson sio makubwa sana, lakini imenilazimu kuchukua tahadhari, ninahofia kama atacheza mwishoni mwa juma hili, huenda akapata majeraha makubwa zaidi, na nikajikuta ninamkosa kwa kipindi kirefu.”
“Keita hana utimamu wa mwili, ninalazimika kumpumzisha”
“Mane amerejea katika hali yake ya kawaida, amefanya mazoezi na wenzake, ninatumai nitamtumia katika mchezo wetu wa leo dhidi ya Red Star Belgrade,” alisema Klopp, ambaye ameshudia vijana wake wakipata ushindi katika mchezo dhidi ya PSG na kupoteza mbele ya SSC Napoli, hali inayoiweka Liverpool kwenye nafasi ya pili katika msimamo wa kundi C.