Meneja wa klabu ya Liverpool Jurgen Klopp anatarajia kukutana na kuzungumza na Washambuliaji Mohammed Salah na Sadio Mane baada ya kusasili mjini Liverpool leo Jumatano (Februari 09).
Washambuliaji hao walikua kwenye majukumu ya kuzitumikia timu za mataifa yao (Misri na Senegal) kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika 2021 (AFCON 2021) zilizofikia tamati mwishoni mwa juma lililopita nchini Cameroon.
Klopp amepanga kukutana na Washambuliaji hao ili kuwasahaulisha na yaliyojiri katika Fainali za AFCON 2021, hasa baada ya kukutana kwenye mchezo wa Fainali na Senegal kuibuka na ushindi kwa changamoto ya mikwaju ya Penati.
Klopp anaamini Mohammed Salah ameumizwa na matokeo ya kupoteza mchezo huo, huku Mane akiwa ni mwenye furaha kwa kuisaidia Senegal kutwaa ubingwa wake wa kwanza wa Bara la Afrika, hivyo anaamini wote wawili wanapaswa kushauriwa ili kuachana na yaliyotokea Afrika.
Wakati huo huo Wawili hao wanatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha Liverpool kitakachoikabili Leicester City katika mchezo wa Ligi Kuu ya England utakaochezwa kesho Alhamis (Februari 10).
Kipindi ambacho Mane na Salah walikua kwenye majukumu ya timu zao za taifa katika michuano ya AFCON, Liverpool ilicheza michezo sita kwenye michuano yote na wameshinda michezo yote ikiwemo michezo miwili ya ligi kuu ya England na pamoja na michezo miwili ya nusu fainali ya kombe la carabao dhidi ya Arsenal.